Mafunzo kwa vikundi vya mikopo ya Halmashauri, Jijini Arusha

Ni mafunzo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya jiji la Arusha na yalifanyika katika ukumbi wa shule ya msingi Arusha, Mafunzo yalilenga vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vitakavyopatiwa mikopo na halmshauri kwa robo ya kwanza na pili mwaka wa fedha 2020/2021. Ambapo vikundi viliwakilishwa na wajumbe 3 kutoka kwenye kila kikundi Mwenyekiti, katibu na mweka hazina kwa jumla ya vikundi 42 vilivyopo ndani ya Halmashauri ya Jiji Arusha.

Mafunzo yalifunguliwa na Mgeni rasmi Titho Cholobi – Afisa tarafa ya Elerai ambaye alimwakilisha Mkuu wa wilaya ya Arusha na alisisitiza vikundi vikafanye miradi yenye tija kwa fedha wanazopewa na serikali na kuzirejesha kwa wakati ili na wengine wenye mahitaji waweze kupatiwa, huku akiwa ametanguliwa na wazungumzaji wengine ambao ni Afisa Vijana – Hanifa Ramadhan alisoma taarifa ya vikundi vilivyopo fedha zilizokopeshwa, zilizorejeshwa, madeni na fedha zinazokusudiwa kutolewa kwa awamu hii, Afisa maendeleo ya jamii jiji – Mwanamsiu Dossi na Naibu meya – Veronica Mwelange. Hawa wote waliweza kuzungumzia juu ya namna serikali ilivyo na nia njema ya kuwasaidia wananchi wake kupitia mikopo hiyo na wakiwahasa watumie fedha wanazopewa kwa maelengo yaliyokusudiwa na sio kuelekeza kwenye matumizi mengine kwa mfano thamani za ndani na kulipa kodi kama walivyozoea wengine

Lengo la mafunzo ilikuwa ni kuwajengea uwezo viongozi wa vikundi ili waweze kuelewa kanuni na taratibu za kusimamia mikopo wanayopatiwa na pia kutimiza wajibu wao kama viongozi. Hivo mada mbalimbali zilifundishwa ambazo ni Uongozi na usimamizi wa miradi, Ujasiriamali na miradi yenye tija, Utunzaji wa kumbukumbu za fedha, Uandishi wa taarifa za mwezi, Urejeshaji wa mikopo na ujazaji mikataba, na Ufugaji wa kisasa. Katika mafunzo hayo  KAKUTE projects tulikuwa sehemu ya wawezeshaji katika mada ya uongozi na usimamizi wa miradi.
Posted in Event.